MNYONGE mnyongeni haki yake mpeni, skandali ya kumbaka na
kumwambukiza Ukimwi mwanafunzi, inamtafuna na kumuumiza Mbunge wa
Urambo Magharibi (CCM), Juma Athuman Kapuya.
Kuhusu ukweli wa skendo hiyo, vyombo vya sheria
vitazungumza lakini gazeti hili limejiridhisha pasipo shaka yoyote kuwa
denti husika ni tapeli na anacheza rafu ili kumharibia Kapuya kwa
maslahi yake.
Gazeti hili, liliamua kumchunguza denti husika ili kumjua
kiundani katika kutimiza ahadi ambayo Global Publishers Ltd, ilishaitoa
kwenye Gazeti la Risasi, nakala ya Jumamosi iliyopita kuwa waandishi
wake watafuatilia kinagaubaga na kuanika kila kitu kupitia magazeti
yake, utekelezaji unaendelea.
HUU NDIYO WASIFU WA DENTI MWENYEWE
Baada ya jana kupitia Gazeti la Ijumaa Wikienda kuzungumza na
Kapuya ambaye alifunguka kila kitu, gazeti hili linaendelea kwa
kumchambua denti husika, wasifu wake na maisha yake yote ya kitapeli.
ANA MAJINA MENGI
Denti huyo amekuwa akijulikana kama Felista, ila anatambulika
pia kama Halima Hamad, hivi karibuni aliamua kujiita Leylat na wakati
mwingine Leila.
Jina ambalo alimuingia nalo Kapuya ili kumtapeli ni Halima
Hamad, upande mwingine hujitambulisha kama Halima Humudi, yaani huchezea
ubini.
MSHANGAO KUHUSU DENTI HUYO
Mwezi mmoja kabla ya sakata la Kapuya halijapamba moto, Felista
alizungumza na waandishi wetu wawili kwa nyakati tofauti, akielezea
uhusiano wake na mheshimiwa huyo ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Miundombinu.
Felista alimweleza mwandishi wa kwanza ambaye ni mwanamke:
“Nina stori kuhusu Kapuya, yule ni mtu wangu, ila subiri kidogo nitakupa
stori kamili.”
Siku mbili baadaye, Felista alimfuata mwandishi wa pili
ambaye ni wa kiume, akamwambia: “Kapuya ananitongoza, ngoja mambo yakae
sawa nitakwambia.”
Hata hivyo, waandishi wetu hawakuingia kwenye mtego huo kwa
sababu mbili. Mosi; si kawaida ya Global Publishers kuandika habari
zenye sura ya upande mmoja kwa maslahi ya mtu, isipokuwa husimamia zaidi
weledi na mizani.
Pili; Felista siyo mgeni kwa waandishi wetu kwa sababu ana
rekodi nyingi za matukio yenye sura ya utapeli, kwa hiyo hakuweza kufua
dafu kuiingiza mkenge Global Publishers.
ENDELEA KUMSHANGAA DENTI HUYO
Baada ya sakata hilo kuibuka kwa nguvu, kasi na ari, waandishi
wetu walimpigia simu Felista kumuuliza ilikuwaje akalifikisha suala
mbali zaidi, huku akijisema yeye ni mwanafunzi wakati siyo kweli?
Felista alimjibu mwandishi wa kwanza: “Huyo aliyepeleka hizo
habari ni Leylat. Mimi Kapuya nafahamiana naye kwa sababu nilishiriki
vikao vya usuluhishi kati ya Leylat na Kapuya. Walimalizana vizuri. Mimi
kama shahidi nilipata shilingi 3,000,000.
“Siku ya kwanza nilipewa shilingi 2,300,000, baadaye alinimalizia shilingi 700,000, tukawa tumemalizana.”
Mwandishi wa pili alipomuuliza, alijibu: “Jamani siyo mimi,
yule ni Leila. Yule mtoto sijui kafikishaje hayo mambo huko, ila mimi
najua kila kitu.”
Baadaye Felista alimpigia simu yule mwandishi wa kiume,
akamwambia: “Kama utanihakikishia pesa ya usafiri nakuja, nitaeleza kila
kitu kwa sababu mimi ndiye shahidi muhimu.”
Mwandishi wetu akambana Felista: “Mimi bado nahisi huyo Leylat unayemtaja ndiye wewe mwenyewe ila unaficha.”
Felista akajibu: “Siyo mimi, halafu sasa hivi sijui mahali alipo ila najua yote kuhusu Leylat na Kapuya.”
Mazungumzo hayo yalifika mwisho, huku Felista akiahidi kufika
ofisi za Global Publishers Ltd, Bamaga, Mwenge lakini baada ya kukata
simu, dakika tatu baadaye alimpigia simu mwandishi wetu, safari hii
akiwa na maelezo haya:
“Nimeongea na Leylat. Amefichwa Maili Moja, Kibaha, Pwani,
hakuna watu wanaoruhusiwa kumuona zaidi ya wanaharakati ambao
wamejitolea kumsaidia kisheria.”
Felista alipotakiwa na mwandishi wetu atoe namba ya Leylat,
alijibu: “Namba hapana ila mkitaka nitawapeleka mkamuone. Yule mtoto
anasikitisha sana, unajua sasa hivi anatumia dawa.”
AKAZUA SEKESEKE OFISINI GLOBAL PUBLISHERS
Jumamosi iliyopita, Gazeti la Risasi likiwa lina uhakika wa
asilimia zaidi ya 95 kwamba Felista ndiye anayecheza sinema yote ya
Kapuya, akibadilisha majina na kujiita mwanafunzi, lilitoa picha yake
kisha likaiziba ili kumtega kisha likamtambulisha kama shahidi muhimu
kama alivyojiita.
Asubuhi mapema siku hiyo, Felista alimpigia simu mwandishi
wetu akilalamika: “Mmeniharibia, Kapuya amenipigia simu anatishia kuniua
kwa sababu anasema mimi nimejifanya kiherehere kwamba najua kila kitu.”
MWANDISHI: Wewe ungekuja ofisini tuongee vizuri.
FELISTA: Sawa nakuja ila lazima muangalie jinsi ya kunilinda, maisha yangu yapo hatarini.
Baada ya takriban saa moja, Felista alifika Global
Publishers na kusema: “Yaani hatari kweli, Kapuya amekuja nyumbani
kwangu, akiwa ameongozana na Leylat. Amesema ataniua kwa sababu mimi
ndiye kiherehere nataka kumharibia.”
MWANDISHI: Kapuya amekuja nyumbani kwako kivipi? Tena akiwa ameongozana na Leylat, mbona unatuchanganya.
FELISTA: Amekuja ndiyo, tena inavyoonekana Leylat mwenyewe sasa hivi yupo pamoja na Kapuya. Ugomvi wao umeisha.
Kapuya anafungua kesi kwa magazeti na mitandao iliyomchafua, Leylat yupo upande wake, mimi nikipingana na Kapuya si nitakufa?
MWANDISHI: Hebu Felista usiongee sana, wewe asubuhi uliniambia
Kapuya alikupigia simu, sasa hivi unasema alikuja kwako, tukueleweje?
FELISTA: Kapuya hakupiga simu, alikuja na Leylat.
MWANDISHI: Inawezekana Kapuya akawa mtoto kiasi hicho? Na kwako alipajuaje?
FELISTA: Mimi sijui, ila pale nyumbani aliletwa na Leylat.
MWANDISHI: Haya tuambie wewe unatakaje?
FELISTA: Nataka pesa ya kodi, nikapange nyumba sehemu nyingine, pale hapanifai tena, nitauawa. Leoleo nataka kuhama.
UWAZI LIKAENDA MBELE ZAIDI
Gazeti hili, lilimuweka ‘pending’ Felista na madai yake kisha
likaingia kazini kumtafuta Kapuya, aweze kueleza wasifu wa denti husika.
“Ni mfupi, mwembamba, mweusi, ana macho makubwa, pua kama
ya Kitutsi, kichwa kirefu,” alisema Kapuya baada ya kukiri kumtambua
msichana huyo anayejiita mwanafunzi.
Kwa kuchambua maelezo hayo, jawabu moja kwa moja lilikwenda kwa
Felista kwa sababu sifa ambazo zimetajwa zinashabihiana naye kwa
asilimia 100.
MWANDISHI: Anaitwa nani?
KAPUYA: Halima Hamad.
MWANDISHI: Mmejuana kwa muda gani?
KAPUYA: Tangu mwaka 2011.
MWANDISHI: Katika kipindi hicho, ulikutana naye mara ngapi?
KAPUYA: Kama mara nne, alikuja kuomba msaada akalipe ada
Tumaini University. Nilimpa shilingi 3,000,000. Awamu ya kwanza nilimpa
shilingi 2,300,000, mara ya pili shilingi 700,000. Nilimsaidia akasome,
sikujua kama ni tapeli.
(Rejea maelezo ya Felista kwamba alipewa shilingi 3,000,000 kwa
awamu mbili. Zilianza shilingi 2,300,000, baadaye zikafuata shilingi
700,000).
MWANDISHI: Ulijuaje kama ni tapeli?
KAPUYA: Kwanza niligundua hasomi na kuna watu alikuwa
anashirikiana nao kunizunguka ili wanitapeli. Nikagundua pia kumbe hata
Mkurugenzi wa CRDB, Dk. Charles Kimei, alimtapeli kwa njia hizohizo.
MWANDISHI: Alikwambia anaishi wapi? KAPUYA: Yule mtoto muongomuongo, kuna kipindi aliniambia anaishi Mbagala, baadaye akasema Gongo la Mboto, hapa juzujuzi, alisema amehamia jirani na Shoppers Plaza.
MWANDISHI: Alikwambia anaishi wapi? KAPUYA: Yule mtoto muongomuongo, kuna kipindi aliniambia anaishi Mbagala, baadaye akasema Gongo la Mboto, hapa juzujuzi, alisema amehamia jirani na Shoppers Plaza.
(Felista aliwaeleza waandishi wetu kuwa anaishi Gongo la Mboto).
MWANDISHI: Namba yake ya simu ni ipi?
KAPUYA: 0713 7…20…0 (tarakimu mbili zimefichwa).
Lengo la kuuliza namba ni kutaka kujua namba aliyonayo Kapuya ili kuifananisha na ile ya Felista ambayo ipo kwa waandishi wetu.
Namba hiyo ndiyo hasa ya Felista, hivyo kuzidi kujidhihirisha kuwa ndiye anayecheza sinema yote.
MWANDISHI: Pamoja na utapeli wake, vipi kuhusu tuhuma za kumbaka na kumuambukiza Ukimwi?
KAPUYA: Jamani sijawahi kubaka katika maisha yangu yote. Sina
Ukimwi. Huyo mtoto anatumiwa na watu kunichafua, maana kuna SMS
alinitumia akaniambia atahakikisha sipati cheo chochote.
TUKARUDI KWA FELISTA
MWANDISHI: Kapuya ameshatufungua na tunajua wewe ndiye mhusika,
FELISTA: Siyo kweli, Kapuya anataka tu kutengeneza mambo ili ajisafishe.
MWANDISHI: Kapuya ametaja namba yako kuwa wewe ndiye mhusika. Na kwa nini ataje namba yako?
FELISTA: Labda kapata namba yangu kupitia kwa Leylat.
MWANDISHI: Kapuya amesema wewe unaitwa Halima Hamad na ndivyo ulivyojitambulisha kwake.
FELISTA: Siyo kweli, mimi naitwa Felista. Hilo jina la Halima silitambui.
(Papo hapo, mwandishi wetu aliiangalia namba hiyo usajili wake
wa laini na Tigopesa na kubaini kwamba jina lililosajiliwa ni Halima
Hamad).
MWANDISHI: Mbona simu yako, laini na Tigopesa, imesajiliwa kwa
jina la Halima Hamad ambalo limetajwa na mheshimiwa? Halima ni nani
sasa?
FELISTA: Turudi kwenye madai ya msingi, msitake kunibadilishia mada?
MWANDISHI: Wewe ndiye Halima, ndiye Felista, ndiye Leylat na Leila. Wewe ndiye unamchezea Kapuya, siyo mwanafunzi, ni tapeli.
FELISTA: Najua mnataka kunichezea mchezo. Mimi siyo Halima.
MWANDISHI: Mbona namba yako umesajili Halima?
FELISTA: Nimesema mimi siyo Halima.
KAMA HUMJUI FELISTA
Felista wa Kapuya ndiye yule binti aliyewahi kumtapeli mke wa
Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma kupitia Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(Wama).
Msichana huyo, alidai yeye ni yatima, akiishi kwa tabu sana,
Mama Salma akaingia mkenge na kumpa kiwanja Mbagala. Baadaye ilipokuja
kujulikana, alishtakiwa kwa utapeli, akapelekwa mahabusu kwenye Gereza
la Segerea, Dar es Salaam.
Felista alikiri kuwekwa Segerea kisha akajitetea: “Kuna watu walitaka kunigombanisha na Mama Salma lakini mbona nilitoka?”
Felista, alishawahi kumuibia marehemu Steven Kanumba kamera,
alipokwenda ofisini kwake, akijidai ni yatima na ana kipaji cha kuigiza,
alipopata mwanya tu, alimliza supastaa huyo ambaye alifariki dunia,
Aprili 7, mwaka jana.
Ukiachana na hilo la Kimei ambalo limetajwa na Kapuya, yapo
matukio mengine ambayo Felista alishayafanya, ikiwemo kudanganya anasoma
alipiwe ada, vitabu, madaftari na sare za shule, kumbe ni ‘gia’ yake ya
kupata fedha kwa njia ya udanganyifu.
SIYO MTOTO KABISA
Uchunguzi wa gazeti hili unalo jawabu kuwa kama kuna uongo
ambao jamii haipaswi kubisa kukubaliana nao ni huu kwamba Felista ana
umri wa miaka 16 na anasoma sekondari.
Gazeti hili limebaini kuwa Felista ni mama wa mtoto mmoja na
lilipombana alikiri: “Ni kweli nina mtoto mmoja, nina umri wa miaka 21.”
Waandishi wetu walifika mpaka Shule ya Sekondari Turiani,
Magomeni ambako alidai anasoma, huko kila mwalimu aliyeulizwa alisema:
“Hakuna mwanafunzi kama huyo anayesoma hapa labda kama mmechanganya
shule.”
Picha na Habari => GlobalPublishers
No comments:
Post a Comment