Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad Anguruma jimbo la Bububu,Ataka wasioitakia mema Zanzibar wasipewe nafasi
Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wafuasi na wapenzi
wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika kiwanja cha Kwa
Geji, kijichi jimbo la Bububu
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Ismail Jussa Ladhu akizungumza na wafuasi
na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika kiwanja
cha Kwa Geji, kijichi jimbo la Bububu.
Wafuasi
na wapenzi wa CUF wakishangilia wakati Katibu Mkuu wa Chama hicho
Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika
kiwanja cha Kwa Geji, kijichi jimbo la Bububu.
Wafuasi
na wapenzi wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif
Sharif Hamad katika mkutano wa hadhara uliofanyika kiwanja cha Kwa Geji,
kijichi jimbo la Bububu.
Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad (katikati), akiwa katika picha ya
pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Ismail Jussa Ladhu (kulia0,
aliyekuwa mgombea wa uwakilishi jimbo hilo Issa Khamis Issa (kushoto),
pamoja na wasomaji wa utenzi mara baada ya mkutano wa hadhara
uliofanyika kiwanja cha Kwa Geji, kijichi jimbo la Bububu.Picha na Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
---
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif amesema watu
wasioitakia mema Zanzibar wasipewe nafasi kuvuruga umoja wa Wazanzibari
ulioimarika baada ya maridhiano ya kisiasa yaliyopelekea kuundwa kwa
mfumo wa serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa.
Amesema
serikali inapaswa kuwa makini na watu hao, na kwamba iwapo viongozi wa
serikali ya umoja wa kitaifa wataendeleza nia njema ya kukuza umoja na
mshikamano, watu hao hawatokuwa na nafasi wala njia ya kupita kupenyeza
matakwa yao dhidi ya umoja wa Wazanzibari.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa kauli hiyo katika viwanja vya Kwa Geji
Kijichi jimbo la Bububu, alipokuwa akizungumza na wafuasi na wapenzi wa
Chama hicho kwenye mkutano wa hadhara, uliolenga kuzunguzia matukio na
matokeo ya uchaguzi wa Bububu uliofanyika hivi karibuni.
Amefahamisha
kuwa Wazanzibari wanapaswa kuwa wamoja katika kutetea maslahi ya nchi
yao, na kuweka wazi msimamo wake wa kutetea muundo wa Muungano wa
Mkataba, ambao itaziwesha nchi mbili zilizoungana kuwa na mamlaka kamili
kwa kila moja, huku zikikubaliana kwa mkataba juu ya mambo ya msingi ya
kushirikiana.
“Mimi
binafsi ni muumini wa Muungano wa Mkataba”, alisisitiza Maalim Seif na
kurejerejea kauli hiyo huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wafuasi na
wapenzi wa Chama hicho waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Amesema
vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa Bububu hivi karibuni
huenda zilipangwa ili kuvuruga umoja wa kitaifa, lakini wenye nia hiyo
hawatofanikiwa kwani wazanzibari walio wengi wameelewa juu ya umuhimu wa
amani na umoja kwa maendeleo ya nchi yao.
Maalim
Seif amewanasihi wazanzibari wanaoitakia mema nchi yao kwa kuweka mbele
maslahi ya nchi badala ya vyama, kutumia changamoto zilizojitokeza
katika uchaguzi mdogo wa Bububu kujipanga katika kutoa maoni kwenye tume
ya mabadiliko ya katiba ili kupata katiba wanayoitaka ambayo itatoa
mwelekeo wa kuwepo kwa mamlaka kamili ya Zanzibar.
Katibu
Mkuu huyo wa CUF alisema ni wajibu wa vyama vya siasa na viongozi
kuelewa kuwa hakuna chama wala mtu mwenye hati miliki ya nchi, bali
wenye mamlaka hiyo ni wananchi wenyewe na kutaka wananchi watendewe haki
na usawa katika huduma zote ninazohusu maendeleo na mustakbali wao.
“Hakuna Chama wala mtu mwenye hati miliki ya nchi hii, nchi hii ni ya Wazanzibari wote kabisa”,alisisitiza.
Alieleza
kusikitishwa kwake na vitendo vya vurugu ambavyo anadai kuwa
vilisababishwa na vikosi vya ulinzi na usalama, na kwamba kufanya hivyo
ni kukiuka maadili ya kazi yao na kuijengea picha mbaya Serikali ya
Umoja wa Kitaifa.
“Mimi
nashangaa sana kwa sababu askari ni wale wale waliosimamia uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010, mbona katika uchaguzi ule walikuwa na nidhamu na
hawakumbumbudhi mtu, inakuwaje katika uchaguzi huu mdogo walete vurugu
na kuwadhalilisha watu?” alihoji Katibu Mkuu huyo wa CUF.
Kwa
mujibu wa taarifa za Chama hicho, watu wapatao 22 walijeruhiwa na
kudhalilishwa wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu uliofanyika
Septemba 16, 2012, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Mtoni Faki Haji Makame
(CUF).
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Ismal Jussa Ladhu
amewataka wafuasi wa Chama hicho Jimbo la Bububu kuwa wastahamilivu
wakati chama kikifuatilia changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo.
Mkurugenzi
wa haki za binadamu, habari, uenezi, mawasiliano na umma katika chama
hicho Salim Bimani, alisema hawakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo,
na kwamba waliotangazwa washindi wanaweza kulitema jimbo hilo, kufuatia
nia yao ya kwenda mahakamani kupinga matokeo yaliyotangazwa.
Katika
risala ya wanachama wa CUF jimbo la Bububu iliyosomwa na bi Mgeni Ali
Suleiman, waliishutumu tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC kwa kushirikiana na
vikosi vya ulinzi kuvuga uchaguzi huo uliompa ushindi mgombea wa Chama
Cha Mapinduzi CCM, na kuonya kuwa hawamtambui na hawatompa ushirikiano
mwakilishi huyo mteule.
Katika
uchaguzi huo, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM Hussein Ibrahim
Makungu alitangazwa mshindi kwa kupata kura 3371 sawa na asilimia 50.7,
dhidi ya mgombea wa Chama Cha Wananchi CUF Issa Khamis Issa aliyepata
kura 3204 sawa na asilimia 48.2
Huu
ni mkutano wa kwanza wa hadhara kufanywa na chama hicho katika jimbo
hilo tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu uliofanyika
Septemba 16, 2012.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar
No comments:
Post a Comment