Tangaza Biashara yako hapa kwa bei nafuu wasilana nasi kupitia 0712 455 139 au 0687 233 209 wote mnakaribishwa. Advertise your Business here at very cheap price Contact us through +255 712 455 139 or +255 687 233 209 your all welcome.

Advertise your Business here at very cheap price Contact us through +255 712 455 139 or +255 687 233 209 your all welcome.
Kikwete anagombea kiti anachokalia, atang'okaje???

Christopher Nyenyembe

KADRI siku zinavyozidi kwenda ndivyo ninavyoendelea kuziamsha hisia za watu kuhusu mchakato mzima wa kampeni za uchaguzi zinavyoendelea,watu wakivutwa na kiu kubwa ya kutaka tarehe ya uchaguzi mkuu Oktoba 31 ingekuwa leo.
Inawezekana uharaka huo wa kutaka kupiga kura kwa maana halisi ya kumpata, Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunatokana na mbinu chafu zilizoanza kujitokeza katika majukwaa ya kisiasa,sauti ya vyombo vya dola na matumizi ya kampeni za kuchafuana kwenye mitandao ya simu, zikionyesha kutumwa toka nchi za mashariki ya mbali.
Hayo ni mambo ya siasa na hakuna mtu anayeweza kubisha au kuzuia moja kwa moja moto ulioenea kwa kasi wa kuchafuana, kutishana na pengine makundi ya watu kadhaa kwa hofu zao na utayari wa kufanya jambo lolote baya kwa lengo la kuwakatisha tamaa wananchi wameibuka sasa.
Sipendi tufike huko nikiamini kabisa kuwa mchakato mzima wa kampeni na lengo mahususi la kufanya uchaguzi mkuu hayo yote yanafanyika kwa matakwa ya wananchi, kwa mujibu wa sheria ya nchi na kikubwa zaidi watanzania wote wana dhamira sawa ya kuhakikisha kuwa wanajenga Taifa lao lenye uongozi imara na lisilokuwa tegemezi.
Viongozi wote waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais hawagombei nafasi hiyo kwa ajili ya kutawala dunia nzima isipokuwa lengo lao kubwa ni kuhakikisha kuwa wanabeba fito imara kwa ajili ya kujenga nyumba moja yenye ustawi wa watu wote watakaoishi ndani yake na hawana sababu ya kugombea fito hizo ili zigeuke fimbo ya kuwaangamiza Watanzania.
Kwa kuelewa hivyo ndio maana nimekuwa na mfululizo wa kutumia karamu yangu kuwaelimisha wapiga kura nikiwa na hamu kubwa ya kuuona uwiano mzuri kwa wagombea wote wa nafasi ya urais kuliko jinsi hali ilivyo sasa ambapo rais aliyopo madarakani ana nguvu ya kuendelea kukikalia kiti cha umma kinachogombewa na wenzake.
Hilo siwezi kuacha kulisema na nikiacha kusema nitakuwa nimepotosha kabisa msingi madhubuti wa makala haya nikiamini kuwa naandika zaidi ili kumgusa, Rais Jakaya Kikwete, mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) anayegombea nafasi hiyo huku akiwa amekalia nafasi ya urais. Hicho ni kitendawili kinachoshindwa kuteguliwa, hata yeye anajua.
Lakini kuna mambo ya msingi na matamko kadhaa ambayo watu makini wanaweza kuyapima kuwa hayaonyeshi ustawi mzuri wa demokrasia ya kweli kwa nchi inayopaswa kuzingatia dhana ya utawala bora, mtu anapokalia mikoba ya Ikulu hadi mwisho wa uchaguzi hakuwezi kuleta tija kwa watu wengine wapenda mageuzi kwani hakuwezi kuleta ushindani sawa wa kisiasa.
Nakumbuka vizuri mwaka 2005 baada ya Rais Kikwete kuapishwa na alipopata nafasi ya kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza, alionyesha ujasiri mkubwa wa kutamka na kupanga mikakati iliyowavutia watu, alionyesha ushawishi wa kutosha huku maneno yake yakisukumwa na ujumbe mzito unaosema, “Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana,” kweli hilo ndio tatizo kubwa la Watanzania.
Watanzania waliamini kabisa toka Desemba 21 mwaka 2005, tayari nyota iliyotakiwa kuwaongoza na kuwaondoa kwenye maisha ya dhiki na tabu ilipaswa kung’ara bila ya kufifia au kuficha makucha makali ndani ya joho la mfalme na baadaye nyota hiyo ilianza kufifia taratibu ikiogopa kuwamulika mafisadi na wezi wakubwa wa mali za umma tofauti na msimamo ulioonyeshwa katika hotuba ya kulihutubia Bunge.
Lakini jambo kubwa linalopaswa kutafsiriwa na wananchi kwa sasa ni nafasi ya urais ambayo watanzania wanaamini kuwa kiti hicho ni mali ya umma na wanatumia nafasi yao ya kupiga kura ili kuweza kumpa uongozi wa nchi kiongozi mwenye uchungu na umasikini huu, hawafanyi hivyo ili kumpata kiongozi anayewaogopa mafisadi hilo hawawezi kulifanya.
Siku zikiwa zinayoyoma, pengine napata shaka ya kuyasema haya yanayohusu nafasi ya rais bila shaka wapo ambao hawajasahau bado kauli iliyotolewa na Kikwete aliyepata ushindi wa kishindo wa asilimia 80 mwaka 2005 pale aliposema “Urais wangu hauna ubia na mtu” hakuna mtu aliyeweza kutafakari kwa undani maana hiyo au kumbishia.
Kuwa Urais wake hauna ubia na mtu,inaweza kabisa ndani ya maneno hayo yakawa na ukweli usiopingika kuwa kiti anachoendelea kukikalia hakina ubia na mtu yoyote ni kiti cha umma alichopewa kwa ridhaa ya wananchi na wananchi ndio wenye jukumu la kumwambia sasa basi au aendelee kukikalia.
Hana kosa amekalia kiti alichopewa kwa asilimia 80 na inawezekana hawa wanaopiga kelele leo wakimtaka akiachie huru kiti hicho ili kiwe wazi kikisubiri rais ajae ni watanzania wachache wasiozidi asilimia 20 ambao mwaka huo hawakumpa kura kiongozi huyo. Inawezekana lakini pamoja na mazingira hayo ipo haja ya kujiuliza kama watanzania asilimia 80 waliopiga kura kwa kishindo mwaka 2005, iweje leo hao hao waonekane kulalamika zaidi huku wakijua kuwa rais aliyopo madarakani ametekeleza ahadi zake kwa asilimia hizo kuwa maisha bora kwa kila mtanzania yamewezekana?
Ameweza kuwashughulikia mafisadi vizuri na ndio maana leo, Rais Kikwete anatamba huku akiwanadi kwenye majukwaa wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM kuwa ni wasafi hata kama kesi zao bado ziko mahakamani na wengine waliojiuzulu kwa tuhuma mbaya, yupo nao na wananchi wanapaswa kuamini watu hao wamesafishwa na rais.
Kimsingi majukumu ya rais aliyekalia kiti hicho hayawezi kusimamishwa na wapiga kura wengi waliojitokeza mwaka huo, lakini pia inawezekana binadamu akageuka kutokana na mazingira kama hayo na katika mafanikio pia inawezekana kundi la watu wachache kwa asilimia 20, ndio walioweza kunufaika zaidi na maisha bora wakawaacha asilimia 80 masikini waliojitolea kumchagua rais wao.
Kwa kipimo hicho, inaonyesha wazi kuwa asilimia 80 ya watu wanaokuwa mstari wa mbele kuchagua viongozi wao, wanafanya hivyo bila ya kuwa na utafiti wowote na ndio hao hao kwa umaskini wao wanaofanikisha kuwapata viongozi wasioweza kukidhi matamanio ya watanzania wote ya kuelea kwenye bahari ya maisha bora.
Kama inawezekana na mara nyingi nimekuwa nikimuona, Rais Kikwete kama Mwanajeshi Mstaafu, Luteni Kanali Kikwete aliyejipambanua kwa mazingira ya kutokata tamaa na kutotaka kushindwa jambo, aliahidi kupambana na wala rushwa kwa nguvu zake zote, kuwajengea watanzania maisha bora na kujenga misingi huru ya soko huria na uwekezaji endelevu bila kusahau alivyotamba kumaliza mgogoro wa kisiasa huko Zanzibari.
Kikwete kwa ujumla wake ni mchumi kitaaluma na naamini kabisa kwa nafasi ya kukalia kiti hicho, angekuwa chimbuko la kuutokomeza umasikini uliopo na kuwa kiongozi mwenye dira na ubunifu mkubwa wa kuwapeleka kule watanzania wanakotaka na kama hayo yametendeka bila shaka yoyote angekuwa rais huru ili apimwe na wagombea wenzake bila kutegemea mamlaka ya umma na nguvu za dola kupata ushindi na kuendelea kukalia kiti.
Awali katika makala yangu ya tano katika mfululizo huu nilitahadhalisha kuwa itakuwa aibu kubwa kwa rais aliyekalia kiti akaondolewa na upinzani kwa nguvu ya umma ile ile iliyomuweka madarakani kwa kuwa hakushituka na kufikiria kuwa kiti hicho kinapaswa kuwa wazi unapofika wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu lakini hilo halionekani, tupo gizani na hilo ndio kosa kubwa la katiba ya nchi.
Nikielekea ukingoni katika makala mbili zijazo, siku 17 zimebaki kabla ya watanzania wote wenye haki ya kupiga kura kujipanga kwenye mistari mirefu ili kuweza kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kumchagua rais wanayeona kuwa atawafaa kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...