WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema shule za msingi hapa nchini zinakabiliwa na
upungufu wa madawati karibu milioni moja na nusu ameitaka Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi ijifunge mkanda na kulipa kipaumbele suala la
kupunguza tatizo hilo.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Mei 3, 2014) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma ambao walihudhuria uzinduzi wa Wiki ya Elimu Tanzania kwenye uwanja wa Jamhuri.
“Takwimu
nilizonazo zinaonyesha kuwa Tanzania ina mahitaji ya madawati 3,302,678
wakati madawati yaliyopo ni 1,837,783 kwa hiyo tuna upungufu wa madawati
1,464,895 katika shule zetu za msingi,” alisema Waziri Mkuu.
Kutokana
na mahitaji hayo, Waziri Mkuu alisema endapo Serikali itaamua
kutengeneza madawati 100,000 kwa mwaka kwa gharama ya sh. bilioni 12/-,
itachukua miaka 15 kumaliza tatizo hilo ili kuziba pengo lililopo sasa.
“Nimepita
kwenye banda la Taasisi ya Maajar Trust na pale wameniambia kuwa
wameshatengeneza madawati 12,000 na kuyagawa katika mikoa sita. Wastani
wa kila dawati ni sh. 120,000/- lakini inategemea na upatikanaji wa mbao
pamoja na gharama za ufundi.”
“Tukichukua
gharama zao, tukaamua kutengeneza madawati 200,000 kwa mwaka,
itatugharimu sh. bilioni 24 na itachukua miaka saba kumaliza tatizo hilo
wakati tukiamua kutengeneza madawati 300,000 kwa mwaka, itatugharimu
sh. bilioni 36 na itachukua miaka mitano kumaliza tatizo hilo,”
alifafanua Waziri Mkuu.
Alisema
ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kumaliza tatizo hilo kwani inatia
aibu na hakuna sababu ya kuendelea kuona wanafunzi wakisoma huku wamekaa
chini.
“Waziri
wa Elimu na watu wako ni lazima mjifunge mkanda na kipaumbele chenu kiwe
ni kupunguza tatizo la madawati katika muda mfupi sana; na itakuwa vema
kama mtajipanga haraka ili mje na suluhisho ndani ya wiki hii kabla
Mheshimiwa Rais hajaja kufunga maonyesho haya,” aliongeza.
"Kaeni na
watu wa Taasisi ya Maajar Trust muone ni kwa njia gani mnaweza kutatua
tatizo hili… kama ni kuandaa chakula cha hisani ili kuchangia madawati
fanyeni hivyo ili tatizo hili liishe. Wako Watanzania wanaweza kuchangia
dawati moja, mawili, matatu au zaidi na tukajikuta tumemaliza tatizo
hili,” alisema.
“Na ninyi
wa TAMISEMI kaeni na kuandaa utaratibu wa kuondoa tatizo hili. Kila
Halmashauri kwa nafasi yake iwe ya mjini au ya vijijini ina uwezo wa
kupunguza tatizo kulingana na fursa ilizonazo. Nasisitiza jambo hili
liwe ni ajenda ya kudumu,” aliongeza.
Wakati huohuo, Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula, akitoa shukrani
kwa niaba ya wadau wa elimu alisema anaunga mkono hoja ya uchangiaji wa
madawati na kusisitiza kuwa kuna haja ya watu kubadili mtazamo walionao
kuhusu suala la uchangiaji wa huduma za kijamii.
“Kuna
watu ukiwaambia kuchangia madawati wanakataa lakini wako waliopokea kadi
nyingi za michango ya harusi na wako tayari kuzichangia kwa sababu
wanajua huko kuna kula na kunywa. Niwasihi wananchi tubadilishe mtazamo
wetu na tuisaidie Serikali katika suala hili la madawati kwa watoto
wetu,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, MEI 4, 2014
No comments:
Post a Comment