JK AZINDUA MTAMBO WA KUFUA UMEME MEGAWATI 60 KUPUNGUZA MAKALI YA MGAO WA UMEME MWANZA.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifunua kitambaa na
kubonyeza kitufe kuashiria kuzindua mradi wa kufua umeme wa megawati 60
huko Nyakato, Mwanza jana. Kushoto ni Waziri wa Nishati na madini
Profesa Sospeter Muhongo. Uzinduzi wa mitambo hiyo ni sehemu ya ufumbuzi wa tatizo la umeme uliokuwa unaikabili kanda ya ziwa.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikagua
mitambo ya kufua umeme wa megawati 60 muda mfupi baada ya kuzindua
mitambo hiyo huko Nyakato Mwanza.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete (kulia akiwa
na mavazi maalumu) akikagua jengo la upasuaji katika hospitali ya
wilaya ya Nyamagana, Mkoani Mwanza.
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
akihutubia maelfu ya wakazi wa Mwanza na miji ya jirani katika viwanja
vya Furahisha jijini Mwanza leo jioni.Rais Kikwete yupo Mkoani Mwanza
kwa ziara ya kikazi kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Maelfu ya wakazi wa Mwanza na miji ya jirani wakimsikiliza Rais Kikwete katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza. (Picha na Freddy Maro).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete jana, Jumapili, Septemba 8, 2013, alizindua mtambo wa
kufua umeme kiasi cha megawati 60 katika eneo la Nyakato mjini Mwanza,
umeme ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza shida ya umeme
katika Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.
Aidha, Rais Kikwete ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza mara moja maandalizi ya
kupeleka umeme kwenye machimbo ya madini ya nikeli yaliyoko Kabanga,
Ngara, Mkoa wa Kagera.
Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake
itaharakisha mipango ya kujenga reli hadi kwenye eneo hilo kama
maandalizi ya kuanza kuchimbwa kwa madini hayo ambayo ni mazito na
kuyasafirisha kwa barabara kwenda bandarini Dar Es Salaam kutaharibu kwa
haraka barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa nchini.
Akizungumza kabla ya kuzindua mtambo huo, Rais Kikwete
ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuharakisha mipango ya kuunganisha
eneo la Kabanga, Ngara, Mkoani Kagera kwenye Gridi ya Taifa ili
uzalishaji wa madini ya nikeli usije kukwamishwa na ukosefu wa umeme.
Amesema kuwa mgodi huo utahitaji umeme mwingi kiasi cha megawati 40.
Rais amesema kuwa Serikali yake itahakikisha inafikisha reli
kwenye eneo la Kabanga mapema ili kuhakikisha kuwa nikeli inayozalishwa
inasafirishwa kwa reli badala ya barabara. Amesema kuwa madini hayo ni
mazito mno na kuyasafirisha kwa barabara kutaharibu kabisa na katika
muda mfupi barabara ambazo zinajengwa nchini kwa gharama kubwa.
Mtambo wa Umeme wa Nyakato wenye uwezo wa kuzalisha megawati
60 ulianza kujengwa mwaka jana, 2012, baada ya Serikali ya Tanzania
kuwekeana mkataba wa ujenzi na Kampuni ya Semco and Rolls Royce ya
Norway mwaka 2011 wakati maandalizi ya ujenzi huo yalipoanza.
Gharama za ujenzi wa mtambo huo ambazo ni shilingi bilioni 130 (Euro milioni 48.7 na dola za Marekani 15.9) zimelipwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza na wananchi kwenye sherehe ya uzinduzi huo, Rais
Kikwete amesema kuwa umeme siyo anasa bali ni moja ya vigezo vya msingi
na muhimu kabisa vya maendeleo.
“Vipo vigezo vingi vya maendeleo ya nchi na binadamu,
lakini moja ya vigezo hivyo ni umeme. Na ukiangalia matumizi ya umeme
kwa kila nchi yanaonesha kiwango cha maendeleo cha nchi hiyo. Katika
Marekani, kwa mfano, kila mwananchi anatumia kiasi cha kilowati 12,000
kwa wastani. Sisi katika Tanzania ni kilowati 89 tu na wastani wa Bara
la Afrika ni kilowati 150,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nc hi yetu ya Tanzania ina umeme kiasi cha megwati 1,450
tu wakati katika Afrika Kusini ni megawati 45,000 na unaweza kuona
tofauti ya maendeleo. Hivyo, ni muhimu sana kwetu kuongeza kiwango cha
kuzalisha umeme katika nchi yetu.”
Katika siku ya tatu ya ziara yake kukagua miradi ya maendeleo
katika Mkoa wa Mwanza, Rais Kiwete pia amefungua Kituo cha Polisi cha
Nyakato ambacho kimegharimu shilingi milioni 450, Serikali ikiwa
imechangia kiasi cha asilimia 20 cha gharama hizo.
Kituo hicho cha kisasa kilianza kujengwa mwaka 2003 lakini
ujenzi wake ukawa unakwamakwama kutokana na ukosefu wa bajeti hadi
uongozi wa polisi wa Mkoa wa Mwanza ulipoamua kukijenga kituo hicho kwa
njia ya kuishirikisha jamii na ikaundwa Kamati ya Ujenzi chini ya
uenyekiti wa Bwana Alfred Wambura.
Akizungumza kwenye sherehe ya ufunguzi wa kituo hicho, Rais
Kikwete ameahidi kuwa atajenga nyumba moja kwa ajili ya makazi ya
polisi. Kituo hicho kina jumla ya askari polisi 65.
No comments:
Post a Comment